UKOSEFU WA VITUO RAFIKI VYA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA
UKIMYA WA WAZAZI JUU KWA WATOTO WAO KUHUSU AFYA YA UZAZI
KUNAPELEKA KUWA NA MAAMBUKIZI YA VVU NA MIMBA ZA UTOTONI KWA VIJANA UMRI KATI YA MIAKA 10- 24
Nakusalimu kwa jina la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania.
Ni matumaini yangu u mzima wa afya ukiwa unaendelea na majukumu yako ya kulitumikia taifa, mimi pia sijambo na ninaendelea na shughuli zangu za kila siku za kuniingizia kipato halali ili maisha yaendelee. Kabla sijakwenda kwenye dhumuni la barua hii, naomba nikupe pongezi kwa yale ambayo umekuwa ukiyasimamia na kutekeleza kama waziri wa afya. Baadhi ya huduma za afya hususani upasuaji wa madaktari bingwa umeimarika ndani ya miaka hii mitatu, hii imetokana na serikali kuwekeza fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba na kusomesha madaktari ndani na je ya nchi. Hapo naomba nikupe maua yako ndugu waziri pamoja na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi bora ya kuwasogezea watanzania huduma bora.
Pia nakupongeza wewe mwenyewe kwa kuwa mwanafunzi bora wa Profesa Janabi, kwakweli unaonekana kufuatilia sana mafunzo yake na umeweza kupunguza uzito. Unaelekea kumrudisha yule Ummy Mwalimu (MB) na naibu waziri wa maendeleo ya jamii wa mwaka 2009.
Ndugu Ummy Mwalimu (MB) na waziri wa Afya, lengo langu kukuandikia barua hii nikukufikishia kilio cha vijana wa umri wa rika balehe (VIJALUNGA). Kilio chao ni kutokuwepo kwa vituo rafiki vya afya na kama kikiwepo basi ni jengo tu ambalo linakosekana upatikanaji wa huduma rafiki za afya kwa vijalunga. Ripoti ya utafiti ya UNESCO inaonesha vijana 52 kati ya milioni 158 wa nchi za kusini mwa Afrika, hupata maambukizi ya VVU kila saa. Maambukizi haya yanaendelea kuwa sababu zinazopelekea vifo vya vijana. Msichana mmoja kati ya watano hupata mimba akiwa na umri wa miaka 17. (chanzo UNESCO)
Takwimu za maambukizi ya VVU kwa Tanzania yanaonesha vijana wenye umri kati ya miaka 10 – 25 ndio wapo kwenye hatari Zaidi yakupata maambukizi mapya. Wakati huo wasichana wapo kwenye hatari Zaidi kuliko wavulana. Inaeleza kuwa maambukizi ya UKIMWI kwa vijana wasio na elimu ni asilimia 6.1, huku wenye elimu wakiwa ni asilimia 0.5. Mchanganuo ni wasio na elimu kabisa (asilimia 6.1), wenye elimu ya msingi (5.5) na waliosoma hadi kidato cha nne (asilimia 2.7). (chanzo TACAIDS)
Vijana wengi wameeleza kuwa vikwazo vya mawasiliano vinazuia upatikanaji wa elimu ya afya ya uzazi kwa kijana.
Changamoto za ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi na vifaa vyake ndio inapelekea matumizi ya vifaa hatarishi kama njia mbadala za kujikinga na tiba. Siku moja kijana wa miaka 17 aliniuliza kuwa matumizi ya vinywaji vya “energy”(vinywaji vyenye kusisimua mwili) kama vinaweza kutoa mimba kwa mwanamke baada ya kushika mimba ndani ya siku mbili.
Mitazamo ya wazazi wengi inapelekea kushindwa kuzungumza na vijana juu ya afya uzazi, kwani wanaamini ukimpa elimu ya afya ya uzazi kwa kijana wa umri kati ya miaka 10 – 19 basi utakuwa umemfundisha kuanza kujihusisha na vitendo vya ngono. Pia kuna vikwazo vingine vidogo vidogo kama vile ukosefu wa maarifa, Lugha za kitabibu zinazotumika, mahli kwa kupata huduma za afya rafiki kwa vijana na upatikanaji wa bidhaa za afya ya uzaza na elimu ya matumizi yake. (kondomu, P2, upandikizaji wa vijiti n.k)
Mheshimiwa waziri, vijana wanaomba kutengenezwa vituo vya afya rafiki kwa vijana kwa ngazi ya kata na tarafa nchi nzima na kuwe na watoa huduma rafiki, kuwatumia viongozi wa kimila na viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kwenye kuhamasisha wazazi wazungumze na vijana wao kuhusu afya ya uzazi ili kupungunza magonjwa ya ngono/VVU na mimba za utotoni.
Pia kuangalia jinsi wizara ya afya kushirikiana na wizara za kimkakati kuwezesha vijana kupata elimu ya afya ya uzazi katika ngazi ya shule. Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, pia ofisi ya waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kuangalia jinsi gani sera za kuthibiti maambukizi ya VVU zinaweza kuwashirikisha VIJALUNGA kwenye kupata elimu, na vifaa mbalimbali vya kuzuia maambukizi ya VVU.
Najua kuna ugumu sana kwenye kutekeleza haya kutokana na mila na desturi zetu ambazo zinasema kuwa kijana haruhusiwi kufanya ngono mpaka atakapooa au kuolewa. Nilifanya mahojiano na vijana kumi kutoka Kilosa na kumi Mvomero, takwimu zilionesha kati ya vijana watano kati kumi wenye umri wa miaka 12-19 tayari wameshafanya ngono na mshirika Zaidi ya mmoja kwa vijana wa kiume. Wakati vijana wa kike wenye umri huo kati ya vijana saba tayari wameshafanya ngono na washirika waliowazidi umri wa miaka 3 mpaka 7.
Takwimu zote hizi zinapatikana, hivyo ukiridhia basi naomba nikuwasilishie mezani kwako ili kuona namna gani serikali sikivu ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaweza kusikiliza kilio cha vijana hawa.
Natanguliza shukrani za dhati kwa kusoma barua yangu hii.
Ni mimi, Gasto